Kwa nini Urusi inawatuhumu wanasayansi wake kwa uhaini?

Anatoly Maslov, Mei mwaka 2024

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Anatoly Maslov, 77, alikuwa naibu mkurugenzi wa taasisi ya kisayansi huko Siberia kwa miongo miwili.
  • Author, Sergei Goryashko
  • Nafasi, BBC Russian

Rais wa Urusi Vladimir Putin mara kwa mara hujigamba kuwa nchi yake inaongoza duniani kwa kutengeneza silaha za hypersonic, ambazo husafiri kwa zaidi ya mara tano ya kasi ya sauti.

Lakini wanafizikia kadhaa wa Urusi wanaofanya kazi kwenye sayansi inayohusiana na silaha hizo wameshtakiwa kwa uhaini na kufungwa jela katika miaka ya hivi karibuni, katika kile ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaona kama ukandamizaji wa kupindukia.

Wengi wa waliokamatwa ni wazee, na watatu sasa wamekufa. Mmoja alichukuliwa kutoka kwa kitanda chake hospitalini katika hatua za mwisho za saratani na alifariki muda mfupi baadaye.

Mwingine ni Vladislav Galkin, msomi mwenye umri wa miaka 68, ambaye nyumba yake huko Tomsk kusini mwa Urusi ilivamiwa mnamo Aprili 2023.

Watu wenye silaha waliovalia barakoa nyeusi walifika saa 04:00, wakichimba kabati na kukamata karatasi zenye fomula za kisayansi, jamaa anasema.

Mke wa Bw Galkin, Tatyana, anasema amewaambia wajukuu wao - ambao walipenda kucheza naye chess - kwamba yuko kwenye safari ya kikazi. Anasema idara ya usalama ya Urusi, FSB, imemkataza kuzungumza kuhusu kesi yake.

Dmitry Kolker

Chanzo cha picha, Familia ya Kolker

Maelezo ya picha, Mtaalamu wa laser Dmitry Kolker alikamatwa kutoka hospitali akiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa wa saratani ya kongosho na alikufa siku mbili baadaye.

Tangu 2015, wanafizikia 12 wamekamatwa na wote wanahusishwa kwa namna fulani na teknolojia ya hypersonic au na taasisi zinazofanya kazi kuhusu teknolojia hiyo.

Wote wanashtakiwa kwa uhaini mkubwa, ambao unaweza kujumuisha kutoa siri za serikali kwa nchi za kigeni.

Kesi za uhaini za Urusi zinafanywa faraghani, kwa hivyo haijulikani wanatuhumiwa kwa nini hasa.

Kremlin imesema tu kwamba "mashtaka ni makubwa" na haiwezi kutoa maoni zaidi kwa sababu huduma maalum zinahusika.

Lakini wenzake na mawakili wa utetezi wanasema wanasayansi hawakuhusika katika utengenezaji wa silaha na kwamba baadhi ya kesi hizo zinatokana na wao kushirikiana waziwazi na watafiti wa kigeni.

Na wakosoaji wanahisi FSB inataka kuunda hisia kwamba wapelelezi wa kigeni wanafuata siri za silaha.

Soma pia:
Ndege ya kivita

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Ndege za kivita zilizobeba makombora ya hypersonic ya Kinzhal ziliruka juu ya Red Square ya Moscow wakati wa gwaride la kijeshi mnamo 2018.

Hypersonic ni makombora ambayo yanaweza kusafiri kwa kasi ya juu sana na pia kubadilisha mwelekeo wakati yakiwa angani, kukwepa ulinzi wa hewa.

Urusi inasema imetumia aina mbili ya silaha hizo katika vita vyake dhidi ya Ukraine - Kinzhal, iliyorushwa kutoka kwa ndege, na kombora la Zircon cruise.

Hata hivyo, Kyiv inasema vikosi vyake vimedungua baadhi ya makombora ya Kinzhal, na kuibua maswali kuhusu uwezo wa silaha hizo.

Muda mfupi baada ya Bw Galkin kukamatwa Aprili 2023, alirudishwa mahakamani siku moja na mwanasayansi mwingine, Valery Zvegintsev, ambaye alikuwa ameandika naye tafiti kadhaa.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali Tass limenukuu chanzo kikisema kukamatwa kwa Bw Zvegintsev huenda kulichochewa na makala iliyochapishwa katika jarida la Iran mwaka wa 2021.

Vladislav Galkin

Chanzo cha picha, Tomsk Polytechnic Institute

Maelezo ya picha, Vladislav Galkin amekuwa kizuizini tangu Aprili 2023, mke wake amewaambia wajukuu wao yuko kwenye safari ya kikazi.

Bw Galkin na Bw Zvegintsev wameangaziwa kwenye makala kuhusu namna ndege za mwendo wa kasi zinavyopenyeza angani iliyochapishwa na jarida hilo.

Katika msimu wa joto wa 2022, FSB iliwakamata wenzake wawili kutoka taasisi moja na Bw Zvegintsev - mkurugenzi wake na mkuu wa zamani wa maabara kwa kazi ya aerodynamics kwa kasi ya juu.

Wafanyakazi kutoka Taasisi ya Nadharia na Mitambo Inayotumika (ITAM) waliandika barua ya wazi kuwaunga mkono wenzao watatu waliokamatwa.

Sasa imeondolewa kwenye tovuti ya taasisi hiyo, ilisema wanajulikana kwa "matokeo mazuri ya kisayansi" na "daima wamebaki waaminifu" kwa maslahi ya nchi yao.

Ilisema kazi waliyoshiriki hadharani imekaguliwa mara kwa mara ili kupata taarifa zilizowekewa vikwazo na tume ya wataalamu wa ITAM - na hakuna iliyopatikana.

Anatoly Maslov, Alexander Shiplyuk, Valery Zvegintsev from  Institute of Theoretical and Applied Mechanics (ITAM)

Chanzo cha picha, ITAM

Maelezo ya picha, Wanasayansi watatu, Anatoly Maslov, Alexander Shiplyuk, Valery Zvegintsev waliandika barua ya wazi kupinga kuzuiliwa kwao.

"Hypersonic ni mada ambayo sasa unawaweka watu gerezani," anasema Yevgeny Smirnov, wakili wa First Division, shirika la kutetea haki za binadamu na sheria la Urusi.

Bw Smirnov aliwatetea wanasayansi na wengine walioshtakiwa kwa uhaini mahakamani kabla ya kuhamia Prague mwaka wa 2021, akihofia athari inayotokana na kazi yake.

Anasema hakuna hata mmoja wa makumi ya wanasayansi hao aliyekuwa na uhusiano wowote na sekta ya ulinzi, lakini walikuwa wakisoma masuala ya kisayansi kama vile jinsi metali inavyoharibika kwa kasi ya hypersonic au athari za msukosuko.

"Hii sio juu ya kutengeneza roketi, lakini juu ya utafiti wa michakato ya mwili," anasema, na anasema kwamba matokeo yanaweza kutumiwa baadaye na watengenezaji wa silaha.

Kukamatwa kwao kulianza na Vladimir Lapygin 83, miaka mika kadhaa iliyopita na alifungwa 2016 lakini akaachiliwa kwa msamaha miaka minne baadaye.

Alikuwa amefanya kazi kwa miaka 46 katika taasisi kuu ya utafiti wa masuala ya anga za juu ya Urusi, TsNIIMAsh.

Vladimir Lapygin

Chanzo cha picha, Bauman Moscow State Technical University

Maelezo ya picha, Lapygin alifungwa gerezani mwaka wa 2016 na kuachiliwa mwaka wa 2020, anasisitiza kuwa hajawahi kutoa taarifa za siri.

Lapygin alipatikana na hatia juu ya kifurushi cha programu kwa hesabu za aerodynamic ambazo alituma kwa mtu wa Kichina. Anasema alituma toleo la onyesho kama sehemu ya majadiliano kuhusu uwezekano wa kuuza kifurushi kamili kwa niaba ya taasisi.

Lakini anashikilia kuwa toleo aliloshiriki halikuwa na taarifa zozote za siri, mfano tu ambao ulikuwa "umefafanuliwa mara kwa mara katika machapisho ya wazi".

Lapygin aliiambia BBC kwamba wote waliokamatwa wakihusishwa na hypersonics "hawana uhusiano wowote na" utengenezaji silaha.

Mwanasayansi mwingine aliyezuiliwa ni Dmitry Kolker, mtaalamu katika Taasisi ya Fizikia ya Laser, pia huko Siberia, ambaye alikamatwa mnamo 2022 akiwa hospitalini na saratani ya kongosho.

Familia yake ilisema mashtaka dhidi yake yalitokana na mihadhara aliyotoa nchini China, lakini maudhui hayo yameidhinishwa na FSB na kwamba wakala alisafiri naye.

Kolker alikfariki siku mbili baada ya kukamatwa akiwa na umri wa miaka 54.

Mabaki

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Mabaki yanayoaminika kutoka kwenye kombora la hypersonic la Kinzhal lililorushwa kwenda Ukraine yalioneshwa kwenye maonesho mnamo mwezi Mei.

"Kuna mzozo ndani ya mfumo," anasema mfanyakazi mwenza wa mmoja wa wanasayansi waliokamatwa, ambaye alitaka kutotajwa jina.

Wanasayansi bado wanatarajiwa kuchapisha kimataifa na kushirikiana na wenzao wa kigeni, "wakati huo huo, FSB inadhani kuwasiliana na wanasayansi wa kigeni na kuandika majarida ya kigeni ni usaliti wa kitaifa," wanasema.

Wanasayansi wa ITAM wanahisi vivyo hivyo. "Hatuelewi jinsi ya kuendelea kufanya kazi yetu," barua yao ya wazi ilisema.

"Tunatuzwa leo ... kesho inakuwa sababu ya mashtaka ya jinai."

Wanaonya kwamba wanasayansi wanaogopa kushiriki katika baadhi ya maeneo ya utafiti, huku wafanyakazi vijana wenye vipaji wakiachana na sayansi.

Barua hiyo ilikuwa mfano adimu wa kuungwa mkono na umma. Taasisi zingine ambazo wanasayansi waliokamatwa walifanya kazi hazijatoa maoni.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi bado ilifanya jaribio la kombora la Zircon kutoka kwenye meli mnamo 2022

Chanzo cha picha, Reuters / Russian Defence Ministry

Maelezo ya picha, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitoa video ambayo ilisema ilionyesha jaribio la kombora la Zircon hypersonic mnamo 2022.

Kesi zingine pia zinasadikiwa kuhusiana na ushirikiano wa kimataifa.

Uchunguzi wa wanasayansi wengine wawili ulihusiana na Hexafly, mradi wa Ulaya wa kuunda ndege ya kiraia ya hypersonic, kulingana na wakili Bw Smirnov, ambaye alishughulikia kesi hiyo.

Mradi huo, ambao sasa umekamilika, uliongozwa na Shirika la Anga la Ulaya na ulianza mnamo 2012.

Shirika hilo liliiambia BBC "michango yote ya kiufundi na kubadilishana mawazo ilikubaliwa na kutabiriwa" katika makubaliano ya ushirikiano kati ya pande za Urusi na Ulaya zinazohusika.

Wanasayansi wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela mwaka jana, ingawa Mahakama Kuu ya Urusi imeamuru kusikizwa upya kwa mmoja wao.

Kukamatwa kwingine kunahusiana na utafiti wa aerodynamics kama gari la anga linaingia tena kwenye angahewa ya Dunia.

Ilifadhiliwa na mpango wa Umoja wa Ulaya na kuendeshwa na Taasisi ya von Karman ya Fluid Dynamics nchini Ubelgiji.

Wachunguzi wa FSB walikuwa na wasiwasi juu ya umbo la koni iliyo na mviringo ambayo ilionekana kama kichwa cha silaha ya kivita katika utafiti ambao mmoja wa wanasayansi, Viktor Kudryavtsev, alituma kwa Taasisi ya von Karman, kulingana na mjane wake, Olga.

Taasisi hiyo inasema mpango huo, ambao ulianza 2011 hadi 2013, "uliondoa wazi kabisa utafiti wa kijeshi". Inasema "haikuweza kupata athari yoyote ya kufichua habari za siri" na timu ya Kudryavtsev.

Mwanasayansi aliyekamatwa Alexander Shiplyuk

Chanzo cha picha, Shiplyuk family

Maelezo ya picha, Alexander Shiplyuk, anayeonekana hapa na mbwa wake Pythagoras, alijitolea maisha yake kwenye kazi yake lakini pia alipenda kuteleza kwenye theluji, mtoto wake anasema.

Makundi ya haki za binadamu yanahisi kuna ukandamizaji unaoendelea.

Bw Smirnov anasema kuwa, katika mazungumzo ya faragha, maafisa wa FSB wamekiri kwake kwamba kesi kuhusu kushiriki siri za hypersonic zilikuwa zikianzishwa "ili kukidhi matakwa ya wale walio juu zaidi".

Anaamini kuwa FSB inataka kutoa hisia kwamba wapelelezi wanawinda siri za makombora ya Kirusi "ili kukabili ubinafsi" wa Bw Putin.

Kesi hizo zinakuja huku kukiwa na ongezeko kubwa la kesi za uhaini.

Sergei Davidis, ambaye anaongoza kazi ya kuunga mkono wafungwa wa kisiasa wa Urusi katika kituo cha haki za binadamu cha Kumbukumbu, anazungumzia "mazingira ya ujasusi na kujitenga", hasa tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.

Akizungumza kutoka Lithuania, ambako shirika lake lilihamia baada ya kupigwa marufuku nchini Urusi, Bw Davidis anasema anaamini kwamba FSB, inapenda kuonyesha kuwa inawasilisha, "huunda takwimu zake za kuripoti kupitia uzushi wa kesi".

Lakini anaamini kunaweza kuwa na sababu nyingine katika kukamatwa kwa wanasayansi, kama vile ushindani wa kandarasi za serikali, au hata ujumbe wa Kremlin wa kutoridhika unaolenga wanasayansi wote wanaohusika katika hypersonics.

Bw Smirnov anasema FSB wakati mwingine hutoa hukumu nyepesi zaidi ikiwa washukiwa watakiri na kuwahusisha wengine.

Kudryavtsev alipewa makubaliano ya kusihi ambayo chini yake angekubali hatia na kunyoosha kidole kwa mtu mwingine, kulingana na mjane wake, Olga.

Alikataa. Alikufa kwa saratani ya mapafu mnamo 2021, akiwa na umri wa miaka 77, kabla ya kesi yake kusikizwa.

Alexander Kuranov akiwa mahakamani

Chanzo cha picha, Mahakama ya Lefortovo

Maelezo ya picha, Alexander Kuranov, aliyepatikana na hatia ya uhaini mwezi Aprili, alikuwa amehusika katika kazi ya kuunda ndege ya hypersonic inayojulikana kama Ajax.

Jenerali Mstaafu wa FSB Alexander Mikhailov anasema FSB "lazima ihakikishe usiri" wa teknolojia ya kijeshi.

Anasema "bila shaka" kwamba lazima kuwe na "sababu kubwa" za hukumu kali kama vile kifungo cha miaka 14 jela kilichotolewa mwezi Mei kwa mmoja wa wanasayansi watatu wa ITAM, Anatoly Maslov.

Jenerali Mikhailov anasema ongezeko la sasa la kesi za uhaini ni zao la kupanuka kwa uhuru na demokrasia katika miaka ya 1990.

Anasema hii ilisababisha mabadiliko ya mtazamo kutoka nyakati za Soviet, wakati anasema wale walio na upatikanaji wa siri za serikali "walichunguzwa kikamilifu" na "kuelewa wajibu" wa kuzifichua.

"Baadhi ya watu walikuwa wakiongea sana na uvujaji ukaonekana," anaongeza.

Kuhusu Bw Galkin, sasa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu mawakala waliofunika nyuso zao wawasili. Jamaa wake anasema alizuiliwa miezi mitatu ya kwanza katika kifungo cha upweke.

Tatyana, mke wake, anasema ana uwezo wa kuzungumza naye kwa simu kupitia sehemu ya kioo na hivi majuzi hata alifikiria kuomba kukamatwa pia "kwa sababu anazuiliwa hapo, siku baada ya siku".

Wanasayansi wengine waliokamatwa nchini Urusi:

  • Alexander Shiplyuk, 57, mkurugenzi wa ITAM, alikamatwa 2022, anasubiri kesi
  • Alexander Kuranov, mkurugenzi wa zamani wa St Petersburg Scientific Research Enterprise for Hypersonic Systems, alikamatwa 2021, alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela Aprili 2024.
  • Roman Kovalyov, mwenzake wa Vladimir Kudryavtsev wa TsNIIMAsh, alihukumiwa kifungo cha hadi miaka saba jela mwaka wa 2020 , alifariki 2022.
Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi