Putin aonya kuwa Urusi inaweza kutoa silaha za kuyashambulia mataifa ya Magharibi

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Putin alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wa kigeni katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa la kila mwaka la St Petersburg

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya kuwa Moscow inaweza kuzipa silaha nchi kwa nia ya kushambulia malengo katika nchi za Magharibi.

Bw Putin alitoa kauli hiyo huku akikosoa hatua ya nchi za Magharibi kuipa Ukraine silaha za masafa marefu .

Nchi kadhaa zikiwemo Marekani zimeipa Ukraine ruhusa ya kushambulia malengo ndani ya Urusi.

Hatua kama hiyo inaweza kusababisha "matatizo makubwa sana," Bw Putin aliwaambia waandishi wa habari wa kigeni.

"Ikiwa mtu anadhani inawezekana kusambaza silaha kama hizo kwenye eneo la vita ili kushambulia eneo letu na kuleta matatizo kwa ajili yetu, kwa nini hatuna haki ya kusambaza silaha za hadhi kama hiyo katika maeneo ya dunia ambako kutakuwa na mashambulizi kwenye vifaa na maeneo muhimu ya nchi hizo?" Rais wa Urusi alisema.

"Hayo ni, majibu yanayoweza kuwiana. Tutafikiri juu ya hilo"

Hakutaja nchi ambazo Moscow inaweza kuzisambaza silaha.

Bw Putin aliitaja Ujerumani, ambayo hivi majuzi iliiambia Ukraine ilikuwa huru kulenga shabaha ndani ya Urusi kwa silaha za masafa marefu zilizotengenezwa na Ujerumani.

"Wanaposema kwamba kutakuwa na makombora zaidi ambayo yatalenga shabaha kwenye eneo la Urusi, hii inaharibu kabisa uhusiano wa Urusi na Ujerumani," Bw Putin alisema.

Rais wa Marekani Joe Biden ameipa Ukraine ruhusa ya kutumia silaha zilizotolewa na Marekani kushambulia maeneo ya Urusi, lakini karibu na eneo la Kharkiv pekee. Ikulu ya White House imesema Ukraine haiwezi kutumia makombora ya masafa marefu ya ATACMS katika ardhi ya Urusi.

Ukraine imetumia silaha za Marekani kushambulia ndani ya Urusi katika siku za hivi karibuni, seneta wa Marekani na afisa mmoja wa nchi za Magharibi aliliambia shirika la habari la Associated Press Jumatano.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kaskazini-mashariki mwa Kharkiv tangu Urusi ilipofanya msukumo katika mpaka wa kaskazini mwa Ukraine. Kharkiv, mji wa pili wa Ukraine, uko kilomita 30 tu kutoka mpakani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Lord Cameron amesema ni uamuzi wa Ukraine kuamua jinsi ya kutumia silaha za Uingereza na kusisitiza kuwa ina haki ya kushambulia maeneo ya Urusi.

Ukraine inasema makombora ya Korea Kaskazini yanatumiwa ndani ya ardhi ya Ukraine, na mashirika ya kijasusi ya Magharibi yanasema Urusi imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran katika mzozo huo.

Unaweza pia kusoma

Urusi ilianzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022.

Bw Putin alikuwa akizungumza na wanahabari wa kigeni katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa la kila mwaka la St Petersburg.

"Kwa sababu fulani, nchi za Magharibi zinaamini kwamba Urusi haitawahi kuzitumia," Bw Putin alisema alipoulizwa na Reuters kuhusu hatari ya kuongezeka ya matumizi ya nyuklia dhidi ya Ukraine.

"Tuna mwongozo wa nyuklia, angalia unasema nini. Ikiwa vitendo vya mtu vinatishia uhuru wetu na uadilifu wa eneo, tunaona kuwa inawezekana kwetu kutumia njia zote tunazo.

"Hili halipaswi kuchukuliwa kirahisi, kijuujuu."

Bw Putin pia alipuuza wazo kwamba Urusi ina mpango wa kushambulia eneo la Nato.

"Hupaswi kuifanya Urusi kuwa adui. Unajiumiza tu kwa hili, unajua?" Bw Putin alisema.

Nani alikuja na hii? Ni upuuzi mtupu tu, unajua?

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah