Nilimtambua dada yangu kwenye video ya wakimbizi waliotekwa vitani Sudan

Luwam Gebru

Chanzo cha picha, Nerayo Ghebru Tesfamichael

Maelezo ya picha, Luwam Gebru alisema wasafirishaji haramu walikuwa wakimpeleka Libya
  • Author, Tesfalem Araia & Netsanet Debessai
  • Nafasi, BBC Tigrinya

Hivi majuzi Mihret Gebru alikuwa akitazama kwa hofu video mbili mtandaoni kwenye simu yake ambazo zilionyesha watu kutoka Pembe ya Afrika wakipigwa na kushambuliwa na watu wenye silaha nchini Sudan - na alishutuka sana kumwona dada yake miongoni mwa mateka.

"Papo hapo niliweza kumtambua Luwam, ambaye alikuwa amejifunika mtandio wa rangi ya chungwa ninayomfahamu vizuri - na viatu vyake, ambavyo vinaweza kuonekana," aliiambia BBC.

Akina dada hao wanatokea Eritrea - na kama vijana wengi Luwam Gebru alikimbia uandikishaji wa kijeshi wa nchi hiyo ambao wanahisi kuwa unawanyima mustakabali wa maisha.

Alikuwa ameishi katika nchi jirani ya Ethiopia mwaka kutoka 2019, ambapo alikuwa na hadhi ya mkimbizi. Lakini kuwa mkimbizi kunaweza kuwa kama kuishi maisha ya kutatanisha - na wengi huamua chaguo hilo hatari kutafuta maisha na fursa mpya.

Bi Mihret alisema nduguye mwenye umri wa miaka 24 aliamua kuhatarisha maisha na kuvuka taifa linalokubwa na vita la Sudan ili kufika Libya mwaka jana, miezi kadhaa baada ya mzozo huo kuzuka.

Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili 2023 wakati washirika wa zamani - jeshi na Wanajeshi wa Vikosi Maalum (RSF) - walianza kupigana wao kwa wao kutaka udhibiti wa nchi.

Raia wengi wa kigeni walihamishwa haraka - lakini baadhi ya wakimbizi ambao tayari wako nchini na wahamiaji waliowasili hivi majuzi kama Bi Luwam walijipata mashakani baada ya kushukiwa na kukamatwa kama wafungwa wa vita.

"Hatukuweza kuwasiliana naye kwa karibu mwezi mzima," asema Bi Mihret.

"Alipiga simu mara moja kutoka Sudan na kutuambia: 'Musiwe na wasiwasi nimefika Sudan na tunaweza kuwasili Libya wiki hii."

Dada yake mdogo alisikika akisema kwa uhakika kwamba watu wanaofanya biashara ya magendo aliowakabidhi maisha yake hawatamumponza.

Lakini hawakupata taarifa zingine kumhusu kwa miezi mingine mitano - hadi video hizo zilipoonekana kwenye mitandao ya kijamii mwezi Aprili.

Pia unaweza kusoma:

Uchambuzi wa BBC Verify wa video hizo unaonyesha kuwa ziliwekwa mtandaoni tarehe 7 na 8 Aprili.

Jenerali wa jeshi la Sudan anawataja wafungwa 50 au zaidi waliokuwa kwenye lori kama "mamluki kutoka Somalia, Eritrea na Ethiopia".

Inaonekana walikamatwa wakikimbia mapigano makali karibu na kiwanda cha kusafisha mafuta cha al-Jaily, kaskazini mwa mji mkuu, Khartoum, ambacho kimekuwa mikononi mwa RSF na kinatumika kama kambi ya kijeshi katika eneo hilo.

Katika moja ya video hizo, afisa wa jeshi anasema mateka hao wanahamishiwa katika kambi ya jeshi ya Wadi Seidna, ambayo pia iko kaskazini mwa mji mkuu.

Kumekuwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba wapiganaji wa kigeni wanatumiwa na RSF - ambayo inaweza kuelezea uhasama wa maafisa jeshi la Sudan dhidi ya kwa kundi hilo

Picha ya mateka wa kigeni wanaoshikiliwa na jeshi nchini Sudan- Aprili 2024

Chanzo cha picha, Social media

Maelezo ya picha, Luwam Gebru, akiwa aliyefunika mtandao wa rangi ya chungwa, akiwa na raia wengine wa kigeni katika picha inayodhaniwa kupigwa mwezi Aprili

Picha ya kundi hilo, ikiwemo Bi Luwam, inaonyesha wakiwa wamejazana kwenye chumba kimoja kwenye ghala.

Bi Mihret, ambaye pia aliweza kumtambua mmoja wa majirani zake kutoka Eritrea miongoni mwa kundi hilo, alisema hawajaweza kupata taarifa zaidi.

"Hatujui mengi, tunaambiwa wako chini ya ulinzi wa mamlaka ya Sudan."

Raia wengine wa Eritrea wameiambia BBC kuwa jamaa zao waliosajiliwa kama wakimbizi nchini Sudan wametoweka na wanaripotiwa kuzuiliwa na jeshi la Sudan.

Wawili kati yao waliondoka Eritrea mwaka jana, na kuwasili katika kambi ya wakimbizi inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa katika jimbo la Kassala mashariki mwa Sudan mwezi Oktoba.

Familia zao zinasema kwamba Yonatan Tesfaslassie, mwenye umri wa miaka 17, na Edmon Kidane, 20, walifikiwa na wasafirishaji haramu.

Wafanyabiashara hao, ambao baadhi yao wanadaiwa kutoka kundi la RSF, mara nyingi huwalenga vijana na wageni wanaowasili nchini humo wakiwaahidi njia salama ya kutoka Sudan kwa ada.

Wakiwa safarini waliwawekea shinikizo la kuwataka jamaa walio nje ya nchi walipe pesa zaidi kisha wawatelekeza njiani.

Bw Yonatan na Bw Edmon kwa mfano, walikuwa wakilenga kuenda Sudan Kusini lakini inaonekana waliachwa njiani na walanguzi na kutengwa.

Wote wawili walikuwa wamefika Wad Madani, katika jimbo la Gezira, jiji lililo karibu kilomita 190 kusini mwa Khartoum ambalo lilikuwa kimbilio salama kwa watu wengi tangu vita vilipoanza.

Lakini mnamo Desemba ulitekwa na waasi wa RSF na zaidi ya watu 300,000 walikimbia eneo hilo kutokana na machafuko hayo.

Hiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa familia ya Bw Yonatan kkuwasiliana naye - aliposema kwamba alikuwa akisafiri na wahamiaji wengine kuelekea Sudan Kusini.

watu wakiabiri lori kutoroka mji wa Wad Madani nchini Sudan - Decemba 2023

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Maelfu ya watu walikimbia Wad Madani kabla ya RSF kuteka jiji la Wad Madani mnamo Desemba

Dada yake Winta Tesfaslassie baadaye alisikia kutoka kwa wale ambao walifanikiwa kuvuka mpaka kwa usalama kwamba huenda ni miongoni mwa wahamiaji wengi ambao walikamatwa katika mji unaoshikiliwa na jeshi wa Rabek kusini mwa Sudan.

Baadhi yao, walisema, walipelekwa katika mji wa karibu wa Sinjah na wengine huenda wakapelekwa katika mji wa Sennar ili kushikiliwa na jeshi.

"Familia nzima ina wasiwasi sana na hatujui la kufanya, tunahisi kupoteza matumaini. Tunataka kujua ikiwa yuko salama, ni mchanga sana kupitia masaibu kama hayo na hana uhusiano wowote na vita vya Sudan,” Bi Winta, anayeishi Uingereza, aliambia BBC.

Familia ya Bw Edmon pia iliwasiliana naye mara ya mwisho alipokuwa Wad Madani - ingawa inaonekana alizuiliwa katika jiji hilo wiki kadhaa kabla ya haujatekwa na waasi wa RSF.

"Tuliambiwa na mfanyabiashara wa magendo kuwa alikuwa anashikiliwa na jeshi la Sudan," dadake Adiam Kidane, ambaye anaishi Angola, aliambia BBC.

Mlanguzi huyo ndiye alikuwa chanzo chao pekee cha habari "lakini baadaye aliacha kupokea simu zetu", alisema.

 Edmon Kidane

Chanzo cha picha, Adiam Kidane

Maelezo ya picha, Msafirishaji haramu aliiambia familia ya Edmon Kidane kuwa kijana huyo alizuiliwa na wanajeshi huko Wad Madani.

"Hatukuweza kumwambia mama yetu kwa muda mrefu lakini hatimaye tulilazimika. Alizimia aliposikia hatuna habari zake. Sote tuko kwenye dhiki.

Baadhi ya ripoti zinasema zaidi ya wahamiaji 200 wa mataifa tofauti walikuwa wamezuiliwa katika kambi ya kijeshi huko Wad Madani kabla ya RSF kusonga mbele - habari ambazo BBC haijafanikiwa kuthibitisha.

Imeripotiwa kuwa wafungwa hao walichukuliwa na jeshi lilipoondoka Wad Madani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema kuwa limepokea ripoti sawia na hizo kuhusu kuzuiliwa na jeshi la wanaotafuta hifadhi na wakimbizi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, kuna zaidi ya Waeritrea 147,000 na karibu Waethiopia 70,000 nchini humo.

Iliambia BBC kuwa inapanga ujumbe wa kuthibitisha katika jimbo la Sennar, ambalo linajumuisha miji ya Sinjah na Rabek, ikiwataka jamaa za wakimbizi wanaoamini kuwa wako kizuizini kuripoti taarifa kupitia ukurasa wa usaidizi wa UNHCR Sudan .

Vile vile Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema wale walio na mwanafamilia aliyepotea nchini Sudan wanapaswa kufungua kesi kupitia nambari yake ya dharura au afisi nchini humo .

"Kusaidia familia ambazo zilipoteza mawasiliano na wapendwa wao kuwatafuta ni moja ya vipaumbele vyetu kuu. Lakini uwezo wetu wa kufanya hivi unategemea uwezo tulionao na hali tete ya usalama,” ICRC iliambia BBC.

Ubalozi wa Sudan mjini London haukujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao kuhusu kuzuiliwa kwa raia wa kigeni.

Licha ya juhudi za kimataifa kusitisha mapigano ambayo zaidi ya watu 15,000 wanaaminika kuuawa, pande zinazozozana haziwezi kukubaliana kusitisha mapigano.

Dada hao watatu ambao wamezungumza na BBC kuhusu ndugu zao waliopotea wanasema ni mchakato wa kufadhaisha sana kupata taarifa zozote ziwe kutoka ICRC, UN au jeshi.

"Tafadhali tusaidie, Umoja wa Mataifa, mtu yeyote ... tumekata tamaa," alisema Bi Winta.

"Tunaziomba mamlaka za Sudan tafadhali, tafadhali waruhusu watuite ili kusikia sauti zao.

"Tunaomba jeshi liwaachilie, hawa ni vijana wasio na hatia ambao waliondoka nchini mwao kwa matumaini ya kufika mahali salama Sudan Kusini."

tt

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi