Haiti yaapa kurejesha utulivu kwa usaidizi wa kikosi kinachoongozwa na Kenya

Na Marina Daras, Gloria Aradi & Pascal Fletcher,

BBC News & BBC Monitoring

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Baada ya miezi kadhaa ya mabishano na changamoto za kisheria bado zinaendelea, Kenya imetuma kikosi chake cha kwanza cha maafisa 400 wa polisi kukabiliana na ghasia za magenge nchini Haiti.

Kutokana na kutikiswa na miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu, taifa hilo la Karibean limeshuhudia kuongezeka kwa ghasia kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moïse miaka mitatu iliyopita.

Makundi hasimu yenye silaha yalichukua udhibiti wa mji mkuu, Port-au-Prince, mapema mwaka huu, na kumlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu wiki kadhaa baadaye.

Magenge yenye silaha sasa yanadhibiti takriban 80% ya jiji.

"Matumizi madhubuti ya nguvu" yanahitajika kukabiliana nao, unasema Umoja wa Mataifa, ambao umeidhinisha ujumbe wa polisi unaojumuisha maafisa 2,500 kutoka mataifa mbalimbali - ikiwa ni pamoja na 1,000 walioahidiwa na Rais wa Kenya William Ruto.

Lakini kuna upinzani mkali nyumbani kwa uamuzi wa Bw Ruto - kwa sababu polisi wa Kenya wanalaumiwa kwa kufanya dhuluma katika nchi yao.

Wakifanya kazi na polisi wa Haiti, na wenye makao yake makuu katika kambi iliyojengwa na Marekani, maafisa wa Kenya watalenga kurudisha maeneo muhimu ambayo yamekuwa chini ya udhibiti wa magenge, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa karibu na bandari za baharini.

Haiti haijafanya uchaguzi tangu 2016.

Kwa hivyo uchaguzi unapaswa kupangwa ndani ya mwaka mmoja, na kuruhusu hilo kutokea, ujumbe unaoongozwa na Kenya unapewa jukumu la kurejesha usalama.

Kutumwa kwao kumeidhinishwa kwa mwaka mmoja, na uhakiki utafanywa baada ya miezi tisa.

Unaweza Pia Kusoma

Polisi wa Kenya watakutana na nini Haiti?

Ghasia za magenge kwa wastani ziliua au kujeruhi zaidi ya mtu mmoja kwa saa katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, kulingana na data ya Umoja wa Mataifa.

Takriban Wahaiti 600,000 wamelazimika kutoka makwao, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji.

Shule na vituo vya polisi katika baadhi ya maeneo vimegeuzwa makazi na familia zinazokimbia ghasia.

Jeshi la polisi la Haiti lina maafisa 9,000 pekee. Kwa upande mwingine inakadiriwa kuwa Wahaiti 8,000 ni wanachama wa magenge 200 au zaidi yenye silaha - na washikilia majukumu kuanzia kuwa makamanda hadi watoa habari. Usajili kujiunga na magenge umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Magenge hayo sasa yana nguvu kubwa sawa na polisi, anasema Emmanuel Paul, mshauri wa usalama ambaye anafanya kazi na makundi ya kibinadamu nchini Haiti.

"Aina mbali mbali za silaha zinatumika na pande zote mbili - bunduki za kivita za aina mbalimbali, AK-47 Kalashnikov za aina mbalimbali," anaiambia BBC.

Rais wa Columbia Gustavo Petro ameshtumu wanajeshi katika nchi yake kwa kuuza makombora na risasi kwa watu wenye silaha, ambao wameziingiza Haiti.

Kwa nini Kenya inafanya hivi?

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makundi ya kijamii katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince yamejulikana kuwa kusambaza mapanga kwa wakaazi

"Tunafanya hivyo kwa ajili ya watu wa Haiti. Jukumu la usalama nchini Haiti ni jukumu la pamoja," asema Bw Ruto.

Lakini wakosoaji wanasema Kenya inafanya tu hivi kuridhisha matakwa ya Marekani na inatumai kupenedelewa na mataifa yenye nguvu, hasa katika masuala ya usalama.

Katika ziara ya hivi majuzi mjini Washington, Bw Ruto pia alitaja kutaka kuinua hadhi ya kimataifa ya Kenya katika ulingo huu.

Kuteuliwa kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa Nato na Marekani bila shaka kumefanikisha hilo.

Lakini nyumbani, Rais Ruto anakabiliwa na upinzani mkubwa na Mahakama ya Kuu ya Kenya imeamua kuwa kutumwa kwa polisi hao ni kinyume cha sheria. Hii ilichelewesha kuwasili kwa maafisa wa kwanza.

Mahakama ilisema kuwa serikali ya Kenya haikuwa na mamlaka ya kutuma maafisa wa polisi nje ya nchi bila makubaliano ya awali ya maelewano.

Makubaliano kama hayo yalitiwa saini tarehe 1 Machi, lakini chama cha upinzani cha Thirdway Alliance Kenya kimewasilisha kesi mpya, kikisema kwamba kutumwa kwa jeshi hilo ni ukiukaji wa sheria.

"Ujumbe huu umeidhinishwa na Umoja wa Mataifa (UN). Ombi hilo lilitoka UN na Marekani. Hakuna ombi la Haiti wala hakuna linaloweza kuwekwa," anasema Charles Midega, wakili wa chama kinachopinga .

"Rais hajafuata utaratibu kama ilivyo kwa katiba ya Kenya na sheria za kupeleka polisi. Na muhimu zaidi, rais hajatangaza Haiti kama nchi inayokubalika kama sharti la kutumwa."

Je, polisi wa Kenya wako tayari kwa misheni ya aina hii?

Ingawa Kenya ina historia ya kushiriki katika misheni za kulinda amani, jeshi lake la polisi halijawahi kukanyaga nje ya Afrika.

Inaaminika kuwa kitengo kilichotumwa kitatoka kwa Kitengo cha (GSU), tawi la polisi ambalo mara nyingi hutumwa wakati wa maandamano na mashambulizi ya kigaidi.

Haijatumiwa dhidi ya mitandao ya kimataifa ya uhalifu kama vile magenge ya Haiti.

Lakini serikali ya Kenya ilisema maafisa waliotumwa walikuwa wamepokea mafunzo maalum, ikiwa ni pamoja na masomo ya lugha ya Kifaransa na Kihaiti ili kurahisisha mawasiliano na wenzao.

Kikwazo kingine kinachoonekana kitakuwa ni utaratibu wa kamandi.

“Kutakuwa na polisi wa Kenya, lakini nchi nyingine zinatuma wanajeshi,” asema Bw Paul.

"Hilo litakuwa jambo la kwanza kuwa changamoto kwa misheni - jinsi ya kuratibu operesheni za polisi na wanajeshi, ikizingatiwa kwamba wana asili tofauti za mafunzo na wana misheni tofauti."

Kamanda mpya aliyeteuliwa Godfrey Otunge atakuwa akiongoza kikosi cha Kenya na atakuwa na kazi nzito mikononi mwake.

Je, polisi wa Kenya wana ufanisi kiasi gani?

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Jeshi la polisi nchini Kenya linashutumiwa kwa ukatili mwingi dhidi ya waandamanaji

Maafisa wa polisi wa Kenya wamekuwa wakikosolewa kwa ukiukaji wa haki za binadamu, na mashirika kadhaa ya haki za binadamu yameelezea wasiwasi wao kuhusu kutumwa kwao Haiti.

Siku ya Jumanne, polisi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, walishtumiwa kwa kutumia risasi dhidi ya waandamanaji wanaopinga kupandishwa kwa ushuru.

Chama cha Madaktari nchini Kenya kilisema kuwa takriban watu watano waliuawa kwa kupigwa risasi,huku idadi ya waliofariki katika vurugu hizo za Jumanne sasa ikitajwa kuwa watu 13 na maafisa wa matibabu.

Bw Ruto aliwatetea polisi akisema maandamano "halali" "yametekwa nyara na kundi la wahalifu waliopangwa."

Katika barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Agosti iliyopita, Amnesty International iliangazia rekodi ya polisi wa Kenya ya kutumia nguvu kupita kiasi.

Pia ilishutumu polisi wa Kenya kwa kuua makumi ya waandamanaji mwaka jana na kuwakamata na kuwaweka kizuizini wengine kinyume cha sheria.

Lakini mkuu wa polisi Japhet Koome alikanusha hili, na mwaka jana alishutumu wanasiasa wa upinzani kwa kuweka miili iliyokodiwa kutoka kwa vyumba vya kuhifadhia maiti katika maeneo ya maandamano ili kuwaulaumu maafisa wake kwa vifo vya waandamanaji.

Je, uingiliaji kati wa hapo awali wa kigeni umekuwaje nchini Haiti?

Haiti imeshuhudia misheni kuu tatu za kulinda amani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, ambazo zimeshindwa kuzuia mzozo huo kuongezeka zaidi.

Mnamo 1994, wanajeshi 25,000 hivi kutoka mataifa ya Karibea walitumwa chini ya operesheni iliyoamriwa na Umoja wa Mataifa.

Miaka kumi baadaye, walinzi wa amani 9,000 wa Umoja wa Mataifa wakiongozwa na Brazil na wanaojulikana kama Minustah walitumwa.

Wakati huu, inaaminika kuwa kikosi kazi kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa kitajumlisha maafisa 3,000 zaidi, ikiwa ni pamoja na wanakandarasi wa raia waliotumwa kwenye nchi hiyo kwa ajili ya usaidizi wa vifaa.

Baraza la mpito la rais wa Haiti hivi karibuni lilimteua Waziri Mkuu wa zamani Garry Conille kuongoza nchi hiyo hadi uchaguzi ufanyike.

Wahaiti wameshuhudia misheni za kulinda amani zikija na kuondoka, bila utulivu kupatikana .

Watakuwa na matumaini ya matokeo tofauti wakati huu.

Ripoti ya ziada ya Natasha Booty

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah